← Back to list

Nafasi ya Utafiti katika Sanaa.

Katika ulimwengu wa sanaa ya kisasa, utafiti mara nyingi hueleweka vibaya kama shughuli ngumu ya kitaaluma au ya kisayansi inayojitenga na…

Ha Bib · 2026-06-16 06:01 · 50 claps · 8.5 min read
#utafiti #sanaa
Open on Medium ↗

Nafasi ya Utafiti katika Sanaa.

Wanafunzi a Nafasi Academy katika somo la Utafiti kupitia Sanaa.

Wanafunzi a Nafasi Academy katika somo la Utafiti kupitia Sanaa.

Katika ulimwengu wa sanaa ya kisasa, utafiti mara nyingi hueleweka vibaya kama shughuli ngumu ya kitaaluma au ya kisayansi inayojitenga na mchakato wa kiubunifu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba utafiti ndio kiini na roho ya uzalishaji wa kazi yoyote ya sanaa yenye uzito. Ni mchakato wa makusudi ambapo msanii huchunguza mawazo, kuelewa mazingira, kuhusiana na jamii, na kuendeleza dhana za kazi yake.

Nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, utafiti umekuwa nguzo muhimu zaidi kadiri wasanii wanavyojibu masuala magumu ya kijamii, kisiasa, kihistoria na kiutamaduni. Wasanii wa kisasa nchini Tanzania hawatengenezi tu kazi kwa ajili ya mapambo ya kuta au burudani ya kupita muda; wanachunguza maisha halisi, kumbukumbu za kitamaduni, utambulisho wa kitaifa na mabadiliko ya kasi ya jamii.

Tunaelewa nini katika dhana ya “Utafiti katika Sanaa”.

Utafiti katika sanaa ni mchakato wa kimkakati wa kutafuta na kukusanya maarifa yanayoongoza na kuratibu uundaji wa kazi za sanaa. Tofauti kubwa kati ya utafiti huu na ule wa kitaaluma au wa maabara ni kwamba utafiti wa kisanaa unajikita zaidi kwenye uzoefu wa hisia, mtazamo wa macho, na majaribio ya kivitendo kwa muundo, hatima au namna ya kisanaa.

Kwa lugha rahisi, utafiti katika sanaa ni uwezo wa kuuona ulimwengu katika jicho la ndani, kuuliza maswali magumu, kukusanya uzoefu wa kibinadamu na kuubadilisha kuwa alama, rangi, sauti, au maumbo ya kisanaa.

Mchakato huu unajumuisha kusikiliza kwa makini hadithi na masimulizi ya jamii, kuchimbua nyaraka za kihistoria, kuangalia maisha ya kila siku ya watu wa kawaida, na kujaribu vifaa na mbinu mbalimbali. Kwa maana hii, kila msanii anayejali ubora wa kazi yake ni mtafiti, iwe ana mafunzo rasmi ya darasani au la.

Lakini, Je! Ni Kwa Nini Utafiti ni Muhimu katika Sanaa?

Linaweza kuwa swali rahisi lakini lenye maana pana ndani yake. Utafiti huongeza uzito na maana ya kazi ya sanaa. Sanaa isiyojengwa juu ya misingi ya utafiti wa kina mara nyingi hubaki kuwa ya juu juu (Uchwara) na hukosa nguvu ya kugusa hisia za mtazamaji kwa muda mrefu.

Utafiti humsaidia msanii kuielewa mada yake kwa upana na undani mkubwa. Kwa mfano, msanii anayeshughulikia suala la uhamaji wa vijana kutoka vijijini kwenda jiji la Dar es Salaam hawezi tu kuchora picha ya stendi ya mabasi. Lazima afanye mahojiano na vijana wa maeneo yasiyo rasmi, achunguze changamoto zao za makazi, na aelewe saikolojia yao. Hatua hii hubadilisha kazi ya sanaa kutoka kuwa taswira ya kawaida tu na kuwa simulizi nzito yenye mguso wa kijamii.

Tanzania ni taifa lenye utajiri mkubwa wa makabila na tamaduni zaidi ya mia moja na ishirini. Katika muktadha huu, utafiti ni zana muhimu ya kuhakikisha tamaduni hizi zinawakilishwa kwa usahihi, heshima na hadhi inayostahili. Msanii anayefanya kazi kuhusu uchongaji wa vinyago vya Mwiko vya kabila la Makonde au chimbuko la muziki wa Taarab kule Zanzibar, lazima aelewe falsafa, muundo, na maana ya kijamii na kihistoria ya sanaa hizo. Bila kufanya utafiti, kuna hatari kubwa ya kurahisisha mambo, kuiga tamaduni za nje, au hata kupotosha utambulisho wa asili wa jamii husika.

Wasanii wa kisasa nchini Tanzania wanabeba jukumu la kuwa vioo vya jamii kwa kushughulikia masuala mtambuka kama vile umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, usawa wa jinsia, ukosefu wa ajira, na changamoto za ukuaji wa miji. Utafiti humwezesha msanii kuvaa viatu vya walengwa. Msanii anayechunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika mwambao wa Tanga au visiwa vya Pemba atalazimika kuzungumza na wavuvi na wakulima wa mwani. Maarifa haya ya nyanjani huleta uhalisia wa pekee na kuifanya kazi ya sanaa kuwa sauti mbadala ya kijamii.

Utafiti wa kisanaa haugusi tu maudhui, bali pia unahusisha majaribio ya vifaa na mbinu za uzalishaji. Kwa mfano, Wasanii nchini Tanzania wanajihusisha na utafiti wa nyenzo kwa kutumia taka zilizorudishwa kwenye mzunguko, mbinu za kiasili za ususi wa mikeka na vikapu, zana za asili za kutengeneza rangi, pamoja na teknolojia mpya za kidijitali na miondoko ya picha. Kupitia majaribio haya yanayotokana na utafiti, wasanii wanagundua lugha mpya za kuona zinazovunja mipaka ya sanaa ya kimapokeo.

Katika zama hizi za utandawazi na mitandao ya kijamii, wasanii wengi wako hatarini kuiga mitindo ya nchi za Magharibi au mataifa mengine bila kuoanisha na mazingira yao. Utafiti unamsaidia msanii wa Kitanzania kupata malighafi ya kipekee kutoka katika mazingira yake ya asili. Hii inamfanya kuwa na saini ya kipekee katika soko la kimataifa la sanaa, ambapo kazi zinazothaminiwa zaidi ni zile zenye utambulisho wa dhati na wa kipekee wa kiutamaduni.

Tumtazame:

Profesa Elias Jengo: Utafiti kama Msingi wa Sanaa

Profesa Elias Jengo anasimama kama nguzo imara na mfano hai wa msanii anayejenga kazi zake kupitia misingi thabiti ya utafiti. Alizaliwa mwaka 1936, na alipata mafunzo yake ya sanaa nchini Uganda, Marekani na Canada, kabla ya kurejea nyumbani Tanzania ambapo alisaidia kuanzisha na kuendeleza Idara ya Sanaa na Maonesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kazi zake za uchoraji na uandishi ni kielelezo tosha cha utafiti wa kina wa kihistoria, kitamaduni na kijamii.

Michoro ya Profesa Jengo mara nyingi inachota msukumo kutoka katika historia ya Tanzania, ikigusa vipindi vya kabla ya ukoloni, wakati wa harakati za ukombozi, na zama za ujenzi wa ujamaa na kujitegemea. Anachunguza kwa kina dhana ya utambulisho wa kitaifa na jinsi maadili ya jamii yanavyobadilika. Kupitia utafiti huu wa kihistoria, kazi zake zimekuwa kama maktaba ya kuona inayohifadhi kumbukumbu muhimu za taifa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Conversation for Whom? (Mchoro wa Prof. E. Jengo)

Conversation for Whom? (Mchoro wa Prof. E. Jengo)

Kazi za Jengo pia zinajikitika katika kuhifadhi mienendo ya maisha ya Kitanzania ambayo iko hatarini kusahaulika kutokana na kasi ya usasa. Hii ni pamoja na taswira za ngoma za kiasili, ala za muziki wa jadi, mandhari ya vijijini, shughuli za kilimo na uvuvi, pamoja na miiko na mila za jamii mbalimbali. Utafiti wake katika maeneo haya unafanya kazi zake ziwe na thamani kubwa ya kianthropolojia, ambapo mchoro mmoja unaweza kusomwa kama kitabu cha historia ya jamii.

Mbali na historia, Jengo hutumia utafiti wake kutoa maoni juu ya masuala yanayoikabili jamii ya sasa, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira, nafasi ya mwanamke katika maendeleo, na athari za kiuchumi kwa wananchi wa kawaida. Kazi zake hazionyeshi tu matatizo, bali zinatumia alama, mafumbo, na taswira zinazomfanya mtazamaji atafakari na kutafuta majawabu ya changamoto hizo.

Mchango mkubwa zaidi wa Profesa Jengo upo katika uwezo wake wa kuhamisha maarifa haya kwa vizazi vipya. Kupitia ufundishaji wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na uandishi wa vitabu na makala za kitaaluma, alihakikisha kuwa wanafunzi wa sanaa hawaishii tu kujua jinsi ya kushika brashi au kuchonga, bali wanaelewa ‘kwa nini’ wanachora au kuchonga. Alihamasisha utafiti wa nyanjani, akisisitiza kuwa msanii lazima awe msomi anayeelewa jamii yake kabla ya kuanza kuishauri kupitia sanaa.

Turejee kwenye mada:

Aina za Utafiti katika Sanaa ya Kisasa Tanzania

Baada ya kuangalia uchambuzi wa sanaa ya Profesa Jengo, sasa Ili kuelewa jinsi wasanii wanavyofanya kazi zao nchini Tanzania, ni muhimu kuangalia aina kuu nne za utafiti wa kisanaa:

  • Utafiti wa kibinafsi: Huu unahusisha msanii kuchimba ndani ya nafsi yake, uzoefu wa maisha yake binafsi, kumbukumbu za utotoni, na hisia zake za ndani ili kupata maana ya mambo yanayomzunguka.
  • Utafiti wa kijamii: Aina hii inahusisha msanii kutoka nje ya studio yake na kwenda kuishi au kushirikiana na jamii. Inajumuisha kufanya mahojiano, muongozo wa madodoso, na uchunguzi wa kina kwa kushiriki ili kupata ukweli wa masuala ya kijamii.
  • Utafiti wa kihistoria na nyaraka: Huu unahusisha kutembelea makumbusho ya taifa, kusoma nyaraka za zamani, kusikiliza masimulizi ya mdomo kutoka kwa wazee wa busara, na kuchunguza picha za kale ili kuelewa chimbuko la jambo fulani.
  • Utafiti wa vifaa, nyenzo na teknolojia: Hapa msanii anajikita maabara au studio kufanya majaribio ya kikemia au kifizikia ya jinsi vifaa tofauti vinavyofanya kazi, kwa mfano, kuchanganya udongo wa maeneo tofauti ya Tanzania na rangi za viwandani ili kuona matokeo yake.

Kuna uhusiano wa moja kwa moja na usiotenganika kati ya utafiti na uundaji wa dhana ya kisanaa. Mchakato wa ubunifu huanza pale msanii anapofanya utafiti, na utafiti huo unapomletea uelewa mpya na wa kina, uelewa huo unabadilishwa na kuwa dhana thabiti ya kisanaa.

Mnyororo huu wa mchakato unaweza kuonekana katika mtiririko ufuatao: msanii anaanza na utafiti, kisha utafiti unaleta uelewa, uelewa huo unazaa dhana, na hatimaye dhana hiyo inatengeneza kazi ya sanaa yenye mashiko.

Bila hatua ya utafiti, dhana za wasanii zinakuwa dhaifu, zenye kukosa misingi, na zisizo na uwezo wa kuhimili mijadala ya ushindani wa kisanaa. Lakini pale utafiti unapowekwa mbele, kazi ya sanaa inakuwa na mizizi miwili: mzizi mmoja katika ustadi wa ufundi na mzizi mwingine katika ukweli wa kijamii na kiakili.

Pamoja na umuhimu huu wote, utafiti katika sanaa nchini Tanzania unakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji ufumbuzi:

  • Ukosefu wa mifuko ya fedha kwa ajili ya utafiti: Tofauti na tafiti za kisayansi, ni nadra sana kupata taasisi zinazofadhili utafiti wa wasanii ili kuwawezesha kusafiri, kukaa vijijini, au kununua nyenzo za majaribio.
  • Mifumo ya elimu inayosisitiza ufundi pekee: Shule na vyuo vingi vya sanaa vya ngazi ya chini vinasisitiza ustadi wa mikono badala ya kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina na kufanya utafiti.
  • Uhaba wa maktaba na hifadhi za nyaraka za sanaa: Wasanii wengi wanakabiliwa na wakati mgumu kupata maandishi au kumbukumbu za kazi zilizofanywa na wasanii wa zamani kama marehemu George Lilanga au Sam Ntiro, jambo linalofanya kila kizazi kuanza upya badala ya kuendeleza pale walipoishia wenzao.

Fursa za Utafiti katika Sanaa Tanzania

Licha ya changamoto zilizoainishwa hapo juu. Bado Tafiti ni msingi imara katia undaji wa sanaa. Licha ya utafiti wenyewe katika sanaa kuwa taaluma au ujuzi wakujitegemea, lakini kuna fursa mbalimbali ziendazo sanjari na utafiti huu katika kumtoa msanii kwenye soko la ndani na kumfikisha katika majukwaa ya kimataifa. Zifuatazo ni fursa kuu tano zilizochambuliwa kwa kina:

  • Makazi ya Wasanii na Ruzuku (Residencies & Grants). Soko la kimataifa linatafuta wasanii wanaozalisha kazi zenye fikra nzito badala ya mapambo pekee. Mashirika kama Goethe-Institut, Alliance Française, na Nafasi Art Space hutoa ufadhili wa masomo, ruzuku ya kifedha, na nafasi za kusafiri nje ya nchi kwa wasanii wanaowasilisha miradi inayotokana na utafiti (research-based art). Utafiti huu unawapa wasanii uwezo wa kushindana na kupata mitaji ya kukuza miradi yao nyanjani.
  • Utalii wa Kitamaduni na Uhifadhi wa Urithi. Watalii na wakusanyaji wa sanaa (art collectors) duniani kote kwa sasa wanatafuta sanaa zenye hadithi na asili iliyothibitishwa. Kupitia utafiti wa kianthropolojia na kihistoria kama vile kuchimbua chimbuko la vinyago vya Makonde, sanaa za miambani Kondoa Irangi, au muziki wa Taarab; wasanii wanaweza kutengeneza kazi zenye nyaraka sahihi. Hii inafungua milango ya ushirikiano na taasisi kama UNESCO, makumbusho ya kitaifa, na hoteli za kitalii zinazothamini sanaa simulizi.
  • Sanaa kwa Maendeleo (Art for Development). Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na mashirika ya kimataifa kama UN na AMREF yanahitaji wasanii kufikisha ujumbe wa kijamii kwa urahisi. Wasanii wanaofanya utafiti wa kitabia katika jamii wanaweza kupata kandarasi nono za kutengeneza sanaa za ukutani (murals), maigizo ya mitaani, au nyimbo maalum ili kuhamasisha masuala ya afya ya uzazi, usawa wa jinsia, na uhifadhi wa mazingira.
  • Maudhui ya Kidijitali na Ushindani wa Kimataifa Katika zama hizi za michezo ya video (video games) na vikaragosi (animations), kuna uhaba mkubwa wa maudhui yenye utambulisho wa Kiafrika. Wasanii wanaofanya utafiti wa ngano za kale, historia, na mavazi ya kiasili wana fursa ya kuuza hatimiliki za kazi zao au kushirikiana na makampuni ya kiteknolojia kutengeneza bidhaa za kidijitali zenye ushindani mkubwa duniani kwa kuwa na vyanzo vya kipekee.
  • Utafiti wa Nyenzo na Sanaa ya Mazingira (Eco-Art). Kutokana na changamoto ya usimamizi wa taka mijini na mabadiliko ya tabia nchi, utafiti wa nyenzo mbadala (material research) unalipa sana. Wasanii wanaofanya utafiti wa jinsi ya kugeuza taka mbalimbli kama vile plastiki, kielektroniki, au miamba kuwa malighafi za sanaa, wananafasi kubwa ya kupata ufadhili ama ushirikiano na mashirika au taasisi ziazojikita na uokoaji wa dunia.
  • Utafiti utakutoa wewe msanii wa Kitanzania kutoka kwenye utegemezi wa kuiga tamaduni za nje na kukupa utambulisho wa kipekee sokoni, hivyo kubadilisha kipaji chako kuwa biashara endelevu na chombo cha mabadiliko.

Utafiti si hatua ya mpito au ya awali tu inayofanyika kabla ya kuanza kufanya sanaa, bali ni sehemu ya mchakato mzima, iliyo endelevu na ya kudumu kwa ubunifu. Wasanii wakubwa na viongozi wa fikra kama Profesa Elias Jengo wamethibitisha kwa vitendo kuwa sanaa inaweza na inapaswa kuwa historia, kumbukumbu ya kiutamaduni, na jukwaa la maoni ya kijamii kwa wakati mmoja. Kazi zake zinaonyesha wazi jinsi utafiti unavyoweza kugeuza sanaa kutoka kwenye burudani rahisi na kuwa chombo chenye nguvu cha elimu na ukombozi wa fikra.

Kwa kuhitimisha mada hii, wasanii chipukizi hapa nchini Tanzania wanapaswa kutambua kuwa utafiti unamaanisha kwamba kila kazi ya sanaa yenye mafanikio lazima ianze na udadisi, ikue kupitia uchunguzi timilifu, na ilete mantiki kupitia tafakari ya kina. Hatimaye, utafiti ndio daraja pekee linalobadilisha sanaa kutoka kuwa usemi wa hisia binafsi za msanii na kuwa chombo kikuu cha mazungumzo mapana, elimu ya jamii, na mabadiliko chanya ya ustawi wa taifa.


메타데이터
post_id
2038b3f2c48b
slug
nafasi-ya-utafiti-katika-sanaa-2038b3f2c48b
url
https://medium.com/@Ha_Bib/nafasi-ya-utafiti-katika-sanaa-2038b3f2c48b
canonical_url
https://medium.com/@Ha_Bib/nafasi-ya-utafiti-katika-sanaa-2038b3f2c48b
author_url
https://medium.com/@Ha_Bib
status
ok
fetched_at
2026-06-24 04:09:36