← Back to list

Maazimio ya Mwaka Mpya — Je, yanaweza kufikiwa?

Kalenda inapogeukia mwaka mpya, kama ilivyo ada, mabilioni ya watu kote duniani husombwa na wimbi au kimbunga cha kujitafakari na…

KOT FM MEDIA_KE · 2025-04-14 09:40 · 0 claps · 5.5 min read
#mwaka-mpya #maazimio #2025 #ndoto #maisha
Open on Medium ↗

Maazimio ya Mwaka Mpya — Je, yanaweza kufikiwa?

Ubao wa maono. Picha kwa hisani ya Akili mnemba (AI).

Ubao wa maono. Picha kwa hisani ya Akili mnemba (AI).

Kalenda inapogeukia mwaka mpya, kama ilivyo ada, mabilioni ya watu kote duniani husombwa na wimbi au kimbunga cha kujitafakari na kujiwekea maazimio ya mwaka mpya yanayoakisi maisha bora na angavu ya siku zijazo. Baadhi ya watu hupendelea kuyarasimu maazimio yao kwenye ubao wa maono au vijidaftari vyao, huku wale wenye tabia ya kutoyatilia maanani wakiyawazia tu akilini au kuyatamania mioyoni mwao.

“Azimio la mwaka mpya ni ahadi tunayojiwekea kuhusu mambo tunayotamani kuyatimiza na au kuyaacha mwaka mpya unapoanza.”

Azimio la mwaka mpya linaweza liwe ni azma ya kununua gari, kujifunza kuogelea, kununua nyumba au uwanja, kufungua au kupanua biashara, kwenda jimu kupiga tizi ili kuondoa kitambi, kujenga afya au kujijengea miraba minne, kuacha pombe, kushika dini, kuboresha mahusiano, kuendeleza masomo, kukata mawasiliano na marafiki wasiofaa, miongoni mwa mambo mengine mengi ambayo tunahisi kuwa yana uwezekano wa kutupa tija kwenye ukuaji wetu kimaisha.

Picha ya mwanadada akiwa kwenye kidimbwi cha kuogelea. Imetumiwa kwa idhini.

Picha ya mwanadada akiwa kwenye kidimbwi cha kuogelea. Imetumiwa kwa idhini.

Swali kizushi hata hivyo ni — je, huwa tunazingatia na kuyatekeleza maazimio haya tunayojiwekea au tunajitutumua tu kwa kuishi katika ulimwengu wetu binafsi wa kiputo wa kujitenga kabisa na uhalisia wa mambo?

Chambilecho wahenga, ni rahisi kusema kuliko ilivyo kutenda, kwani mara nyingi huwa tunashindwa kuyatekeleza maazimio kwa sababu moja au nyingine.

Mimi binafsi kama ilivyo desturi, kila tunapovuka mwaka, azma yangu huwa kuwa kiumbe bora zaidi kuliko mwaka uliopita — kwenye kila nyanja ya maisha yangu na kwa wanaonizunguka. Kwa mfano, ujio wa UVIKO-19 na kusitishwa kwa shughuli za kawaida kulikotokana na janga hilo (2020 hadi 2022) kulinipelekea kuwa na azma ya kujifunza lugha za kigeni na lugha asilia za nchi za Kiafrika, hatua iliyonifanya niboreshe Kireno changu cha Kibrazili kwa kiasi kukubwa, nijifunze Shikomori (lugha inayozungumzwa visiwa vya Komoro), Kibambara (lugha inayozungumzwa nchini Mali), miongoni mwa lugha nyingine za asili.

Mwaka wa 2024, azma yangu ilikuwa ni kuuvukia mwaka nchini Tanzania, kuzuru sehemu za historia zinazohusiana na ukoloni na au vita vikuu vya dunia kama vile Longido, makaburi ya Polandi Arusha, kanisa la Akeri Tengeru, na mji adhimu wa Bagamayo. Haya yote niliweza kuyatiki kwenye orodha yangu ya matamanio. Hata hivyo, kuna mengi pia ambayo sikuweza kuyatimiza mfano kuwa mwandishi wa mara kwa mara katika jarida moja la Kiswahili nchi jirani (jina nimelibana) na mengine makuu ambayo ni binafsi kwangu.

Mwaka huu wa 2025, labda kidogo niige ile video ya kuchekesha ya mtandaoni (*meme*), ya aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara almaarufu ‘Bwege’, ninajipa motisha kwa kukiri kuwa “ninaanza upya!”. Yale niliyoshindwa kuyatekeleza ndani ya mwaka wa 2024,nitajitahidi insha’Allah kuyatekeleza ndani ya 2025 nikianzia na uandishi wa haya makala ya Kiswahili unayoyasoma, japo kwenye jarida tofauti la hilo nililoelezea hapo juu.

Ingawa ibada hii ya maazimio ya kila mwaka imesalia kuwa sehemu ya jamii kotekote duniani,hakuna takwimu maalum barani Afrika kuhusu ni Waafrika wangapi hufanya maazimio ya Mwaka Mpya na kuyafikia. Hata hivyo, baadhi ya marafiki zangu wa karibu, na Wana Afrika Mashariki kwa jumla niliopata kuhojiana nao walikiri kushiriki utamaduni huu kwa kufanya maazimio fulani mahsusi ya kibinafsi. Mdahalo uliweza kubaini kuwa kwa wastani, kupiga dili za kishua zenye kitita kikubwa cha pesa kulipewa kipembelezo. Katika ngazi za kimataifa, utafiti wa mtandao wa InsideOutMastery unaonyesha kuwa asilimia 38.5 ya watu wazima nchini Marekani huweka maazimio ya mwaka mpya kila mwaka, huku asilimia 52.6 ikizingatia angalau azimio moja la mwaka mpya, na asilimia 47.4 ikizingatia maazimio zaidi. Vilevile utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 59 ya vijana kati ya miaka 18 na 34 hujiwekea maazimio hivyo kulifanya kundi hili kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wenye maazimio ya mwaka mpya.

Hata hivyo, utafti uanonyesha kuwa watu wenye umri zaidi ya miaka 55 walibainiwa kuwa na uwezekano mdogo sana wa kuweka maazimio mara 3.1 chini zaidi ikilinganishwa na watu wazima wenye umri mdogo. Hii ina maana kwamba kadri mtu anavyopanda umri, ndivyo anavyosheheni uwezekano mdogo wa kuwa na maazimio ya mwaka mpya. Hali hii japo ni tofauti kwa wazazi walio na watoto, kwani asilimia 54 wanasemekana kuwa na maazimio ya Mwaka Mpya, ambayo ni mara 1.6 zaidi kuliko wale wasio na watoto.

Je, maazimio ya mwaka mpya hudumu kwa muda gani, na mbona watu wanafeli pakubwa kuyafikia?

Utafiti unabaini kuwa takriban asilimia 43 ya watu wanatarajia kushindwa kuzingatia maazimio ya mwaka kabla ya mwezi wa Februari, huku asilimia 23 ya watu wakishindwa kuyazingatia baada tu ya wiki ya kwanza ya Januari, asilimia 64 baada ya mwezi wa kwanza, na asilimia 81 kabla ya mwisho wa mwezi wa pili. Aidha, asilimia 43 ya watu wanatarajia kukata tamaa kufikia malengo yao ifikapo Februari, hali ambayo inaelezea kiwango cha juu cha kushindwa ndani ya Januari. Kinachoshangaza, ni asilimia 9 tu ya watu ambao wanasemekana kufaulu kutimiza maazimio yao ya mwaka mpya.

Basi iweje kwamba wengi wetu tuna ari ya kuweka maazimio, lakini tunashindwa na safari ya kuyatimiza baada tu ya wiki ya kwanza au ndani ya mwezi wa kwanza wa mwaka mpya? Mfano murua ni wa wale wenye mazoea ya kujimwambafai na kujitia mashobo na ratiba kali za jimu. Inapotinga Januari, pitiapitia jimu za mitaani, utakuta zimefurika furifuri — na mabanati wanaolenga kujipatia shepu na viuno vya nyigu, pamoja na wakaka wenye vitambi wanaolenga kuvipunguza, kujenga vifua, miraba minne na misuli tinginya. Kwa kawaida, wamiliki wa jimu wanasemekana kutabasamu hadi benki kwa vile wanajivunia hela chungu nzima nyakati kama hizi kwa sababu wanaojisajili huongezeka maradufu. Hata hivyo, tabasamu zao hukatizwa ghafla na mambo kuanza kuwaendea segemnege pale wanajimu wao wanapokata tamaa na kuanza kusepa mazoezi makali.

Kiuhalisia, inabainika kuwa sababu kuu ya maazimio ya watu kufeli ni pamoja na kukata tamaa au matumaini na kile walichoapa kukitimiza, na vilevile kuweka maazimio na matarajio ambayo hayawezi kutekelezwa au kufikiwa.

Sijui wewe kama msomaji wa makala haya ya umepanga kutimiza jambo lipi mwaka huu wa 2025. Huenda umeazimia kuzingatia afya yako ya akili, kutimiza ndoto yako ya kitaaluma, kusafiri nje ya nchi yako ya asili, kununua “ndinga ya kishua” kama wanavyosema wanamitaani,kuuasi ukapera, kuacha kupiga mtindi au soda,na kingine kile unachokiazimia. Cha kuzingatia ni kujitahidi sana kuwa mwenye nidhamu na wa kujituma iwapo ungependa kujumuishwa kwenye takwimu za wale watu ambao watafaulu kutimiza maazimio yao ya mwaka huu mpya.

Konfusio (Confucius kwa lugha ya King’eng’e), mwanafalsafa mashuhuri wa Kichina wa karne ya tano KK aliwahi kusema “Inapodhihirika kuwa malengo hayawezi kufikiwa, usirekebishe malengo, bali rekebisha hatua zako”. Kuepuka kukata tamaa na maazimio yako ya Mwaka Mpya, zingatia maneno haya kuntu ya mwanafalsafa huyu na bila shaka utafika mbali na azma yako. Kwa hiyo, ikikulazimu, rekebisha hatua ya kufikia malengo hadi hatua ya “SMART”, yani hakikisha kuwa Ni Mahususi, Yenye kupimika, Inayoweza Kufanikiwa, Inayofaa, na Iliyowekewa Muda fulani.

Lakini pia chukua tahadhari ya kuepuka kiputo na mafanikio mahususi makuu ambayo mara nyingi yanaweza kukupelekea kupata shinikizo linalotokana na kuhangaishwa na jitihada za kufikia malengo hayo mahsusi ya dau kubwa ulilojiwekea.

Isitoshe, katika safari yako, zingatia ya kwamba hakuna chenye thamani kijacho kwa njia rahisi — lazima uweke juhudi ili kupata kufikia chochote kile unachokitamani maishani.

Kuhitimisha, usishindane na yeyote yule, kwani kila mtu ana safari yake ya kipekee ambayo haiwezi kulinganishwa na ya mtu mwingine. Na muhimu zaidi, usisahau kanuni ya “kila hatua, D’ua.”

Nikutakie heri na fanaka tele kwenye kufikia maazimio yako ya mwaka huu wa 2025!

Imeandikwa na: Ripota wa Kot FM

Ilani: Maoni yaliyotolewa katika makala haya ni yale yaliyokusanywa na mwandishi na huenda yasiakisi mtazamo ya KOT FM Media na au huluki zake zozote zinazohusiana kwa vyovyote vile.

Kwa kuwa uko hapa…

KOT FM hufanya kazi kama jukwaa linaloendeshwa na jamii, ikiweka kipaumbele ukweli, uwazi, na mazungumzo yenye kujenga. Tumejengwa juu ya imani kwamba uandishi wa habari huru, unaojenga na unaoendeshwa na watu ni muhimu. Kwa hivyo, tunawaalika wale wanaoshiriki maadili haya kuchangia ruwaza yetu.

Kwa kuunga mkono kazi yetu, unawekeza katika utoaji habari usiovurugwa, wa ukweli, na wenye matokeo na kuwezesha mazungumzo muhimu ambayo yanawezesha jamii ya mtandaoni nchini Kenya kuleta mabadiliko chanya.

Ili kuunga mkono maudhui yanayofahamisha, kuhusisha na kuwezesha jumuiya ya maarifa, tafadhali tuma ahadi yako ya mchango kwa barua pepe kotfm.media[at]gmail.com na tutafuatilia na maelezo kuhusu jinsi mchango wako utakavyotumiwa.

“Azimio la mwaka mpya ni ahadi tunayojiwekea kuhusu mambo tunayotamani kuyatimiza na au kuyaacha mwaka mpya unapoanza.”


메타데이터
post_id
226f7ebdbbce
slug
maazimio-ya-mwaka-mpya-je-yanaweza-kufikiwa-226f7ebdbbce
url
https://medium.com/@kotfm.media/maazimio-ya-mwaka-mpya-je-yanaweza-kufikiwa-226f7ebdbbce
canonical_url
https://medium.com/@kotfm.media/maazimio-ya-mwaka-mpya-je-yanaweza-kufikiwa-226f7ebdbbce
author_url
https://medium.com/@kotfm.media
status
ok
fetched_at
2026-07-20 08:03:32