#MpendwaDrSalim
Leo Tarehe 23.1.2022 Balozi mashuhuri na Waziri Mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim anatimiza miaka 80, sijawahi kutana nae ila nimevutiwa…
#MpendwaDrSalim
Leo Tarehe 23.1.2022 Balozi mashuhuri na Waziri Mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim anatimiza miaka 80, sijawahi kutana nae ila nimevutiwa sana na historia ya maisha yake baada ya kumsoma kwenye vitabu na makala mbali mbali.
Dk Salim Ahmed Salim anaweza kuelezewa kwa njia nyingi. mwanadiplomasia mashuhuri, mwanadiplomasia wa kimataifa, mtetezi wa demokrasia, mwanasiasa shupavu na mahiri, mwanamapinduzi, mwanasiasa wa Kiafrika na mwana Pan -Africanist aliyejitoa kwa watu wa Bara la Afrika

Picha ya Dk Salim Ahmed Salim
Maisha yake ya kisiasa yalianza akiwa na umri wa miaka 17 aliposaidia kuanzisha na kuongoza kikundi cha wanafunzi mahiri cha “All Zanzibari National Student Organisation.” Baadaye akawa kinara ndani ya harakati za ukombozi wa Wazanzibari akiwa na umri huo alikutana na Mwl.Nyerere.
Pia akiwa mhariri wa gazeti la chama cha Umma Salim aliweza kuwa na mchango mkubwa katika kuwatia moyo wananchi wa Zanzibar katika harakati zake za kupigania uhuru kutoka kwa ukoloni wa Waingereza.
Baada ya mapinduzi ya 1964 yaliyopelekea kupinduliwa kwa Sultani na serikali yake, Rais Abeid Karume wa Zanzibar alimteua Salim kuwa Balozi wa Zanzibar huko Cairo akiwa na umri wa miaka 22 tu.

Kwenye picha akikabidhi hati ya utambulisho kwa Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri.
Akihojiwa na Hamza Kasongo mwaka 2018 alieleza namna alivyokuwa anamuelezea Mzee Karume kuwa nafasi aliyoipata ni ngumu kwake kwani hana uzoefu wa kutosha ila Rais Karume alimjibu “Kwani mimi nilijifunza kuwa Rais”
[embed]
Mwaka 1971 akiwa mwakilishi wa Tanzania kama Balozi wa Umoja wa Taifa alikuwa mstari wa mbele wa kuitetea China kuwa mwananchama wa Umoja huo,viongozi wengi wakubwa walimtumia barua za vitisho za kumtaka ‘akae kimya’ ila jambo hilo halikumteteresha alisimama kidete.
Barua ya vitisho aliyotumiwa Dk. Salim Ahmed Salim na mjumbe mmoja wa Baraza la Umoja wa mataifa mwaka 1971.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa ya Kuondoa Ukoloni Duniani, Dk Salim alikuwa mahiri kuibua enzi mpya ya uhuru katika bara zima la Afrika.
[embed]
Akiongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Vikwazo dhidi ya Rhodesia, Rais wa Mkutano wa Kimataifa wa Vikwazo dhidi ya Afrika Kusini na Rais wa Mkutano wa Kimataifa wa Paris kuhusu Ubaguzi wa rangi. Kwa kutambua mchango wake kwa Afrika ametunukiwa tuzo nyingi za kitaifa kutoka safu ya nchi za Afrika, zikiwemo Togo, Rwanda na Liberia.
Maisha ya uongozi ya Dk. Salim yanatukumbusha kuwa utetezi wa wanaonewa ni muhimu na pengine katika hali yoyote ile unapokuwa na nafasi ya kuwa mmoja wa kuwafanya wawe na amani basi kutimiza majukumu yako sio ombi bali ni takwa la nafasi uliyonayo.

Dk. Salim Ahmed Salim akiwa na kiongozi wa zamani wa taifa la Cuba Fidel Castro
Umahiri huo aliowahi kuuonesha katika nafasi alizowahi kuzishika zinadhirisha kuwa alikuwa tu sio kiongozi wa Tanzania bali Afrika yote, hata leo akiwa anashereherekea miaka 80 viongozi wa Afrika wamejitokeza kuonesha furaha waliyonayo juu yake, kupitia mtandao wa Twitter na hashtag ya #DearDrSalim
메타데이터
- post_id
- 4e8a0f4cb495
- slug
- mpendwadrsalim-4e8a0f4cb495
- url
- https://medium.com/@msafir/mpendwadrsalim-4e8a0f4cb495
- canonical_url
- https://medium.com/@msafir/mpendwadrsalim-4e8a0f4cb495
- author_url
- https://medium.com/@msafir
- status
- ok
- fetched_at
- 2026-07-27 14:41:33