← Back to list

Ukweli Mgumu Kuhusu Upendo na Ndoa Watu Wengi Huujua Wakiwa Wameshachelewa

Upendo Ni Mwanzo, Siyo Msingi

Sandrahope Msigwa in Love Shack · 2025-04-22 13:43 · 50 claps · 5.0 min read
#swahili #mapenzi #ndoa #upendo #familia
Open on Medium ↗

Ukweli Mgumu Kuhusu Upendo na Ndoa Watu Wengi Huujua Wakiwa Wameshachelewa

Upendo Ni Mwanzo, Siyo Msingi

Kama umewahi kupenda, unajua hisia zake: hisia za furaha, meseji za usiku wa manane, kutamani kuwa pamoja kila wakati, na hisia ya furaha unapomsikia mpenzi wako. Wengi wetu tumekua tukiamini hadithi hii ya kimapenzi: “Tukipendana, basi inatosha.”

Huo ni ule wakati changa wa kimapenzi katika uhusiano, na kama alivyoeleza Dkt. Gary Chapman katika kitabu chake Things I Wish I Knew Before I Got Married, huu ni wakati wa mapenzi ya mwanzo — hisia za mvuto, shauku, na matarajio. Ni halisi, lakini pia ni wa muda mfupi. Wakati huu ni wa mtego mkubwa kwa wanaochukua maamuzi makubwa kama kuoa/kuolewa kwa misingi ya hisia hizo. Kwa sababu, maisha halisi huibua ukweli ambao unaweza kuokoa ndoa nyingi hata kabla hazijaanza: Upendo peke yake hautoshi.

Utafiti unaonyesha kuwa mapenzi hayo ya awali hudumu wastani wa miaka miwili. Baada ya hapo, maisha huanza — msongo wa mawazo, bili, kazi, migogoro, na matarajio yasiyotimizwa.

Hapo ndipo mahusiano huvunjika au huingia katika hatua ya juu zaidi: upendo wa makusudi (intentional love).

Aina ya upendo inayokupeleka kwenye ndoa, siyo aina ya upendo itakayokuweka ndani ya ndoa.

Wakati changa wa kimapenzi yanaisha, upendo wa makusudi unachukua nafasi. Huu ni upendo unaochaguliwa kila siku, unaodhihirika kwa matendo ya kujali na kujitolea. Ni upendo unaosema, “Hata siku nisipojisikia, bado nitakuwepo. Bado nitakuchagua.”

Upendo wa makusudi husikiliza wakati wa kutofautiana, hujitolea hata wakati wa uchovu, husamehe hata kama ni vigumu, na hujitahidi kuelewa na kuhudumia mwenzi wake. Haujitokezi tu — unajengwa, hatua kwa hatua, kwa jitihada za kweli.

Kuingia kwenye ndoa kwa msingi wa mapenzi changa ya kimapenzi ni kama kuanza safari ya barabarani ukiwa na nusu ya mafuta. Mwanzoni ni raha, lakini bila maandalizi na vifaa sahihi, safari itakwama.

Ndoa inahitaji zaidi ya hisia. Inahitaji ukomavu wa kihisia, mawasiliano ya kina, mbinu za kutatua migogoro, na maadili yanayofanana. Bila hayo, hata wapenzi waliopendana sana wanaweza kushindwana.

Dhana ya “Upendo Unatosha” Ni Hadithi Tu

Marafiki zangu Adam na Angel ni mfano halisi. Walikutana, wakapendana mara moja, na baada ya wiki moja wakaanza kuambiana “wewe ndiye wangu wa maisha.” Miezi minane baadaye, walifunga ndoa. Kwa nje walionekana kamilifu — matembezi ya kimapenzi, picha tamu za Instagram, na sherehe kubwa ya harusi.

Lakini baada ya harusi, uhalisia ulianza kujitokeza. Hawakuwa wametumia muda wa kutosha kujifunza namna ya kushughulikia tofauti zao, kuelewa hali za kihisia za kila mmoja, au hata kupanga malengo ya muda mrefu. Walianza kubishana zaidi ya kuungana. Tofauti ndogondogo walizoziona wakiwa wachumba zikawa vyanzo vikuu vya msongo ndani ya ndoa.

Walikuwa bado wanapendana — lakini ukweli ukajitokeza: upendo peke yake haukuweza kubeba uzito wa maisha ya kila siku.

Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Kufunga Ndoa

Haya ni baadhi ya maswali na maeneo muhimu ambayo wanandoa wajao wanapaswa kuyajadili kwa kina kabla ya kusema “ndiyo.” Majibu yake yanaweza kuonyesha kama mna msingi thabiti au mnategemea bahati tu.

Je, tunajua kushughulikia migogoro vizuri?; Kila wanandoa hugombana. Swali ni kama mnalenga kuelewana au kushindana. Je, mwenza wako husikiliza? Hujiweka kando au hufoka? Jifunze kutatua migogoro bila kudhalilishana, hii ni moja ya kitu muhimu sana kwenye mahusiano.

Mtazamo wetu kuhusu fedha ukoje?; Pesa huathiri kila sehemu ya ndoa — bili, akiba, matumizi, madeni. Je, mnaelewana kuhusu bajeti na malengo ya kifedha? Zungumzeni wazi kuhusu fedha kabla ya ndoa.

Je, mnaendana kiroho?; Si lazima muamini sawa, lakini mtazamo wa kiroho huathiri maamuzi, malezi, vipaumbele. Je, mnaweza kuheshimu na kusaidiana katika imani zenu? Imani kwenu ikoje katika maisha ya kila siku?

Je, mnajua lugha ya mapenzi ya kila mmoja?; Watu hupokea na kuonyesha mapenzi kwa njia tofauti — maneno, kuguswa, huduma, zawadi, au muda wa pamoja. Kujua lugha ya mapenzi ya mwenza wako huongeza uhusiano kwa kina.

Matarajio yenu kuhusu majukumu ya ndoa yakoje?; Nani hupika? Nani hulipa bili? Nani hupanga matembezi au kuwasiliana na familia? Kuzungumza haya mapema huzuia chuki baadaye. Pia kumbuka majukumu yanaweza kubadilika huko mbeleni mtaweza kubadilika?

Je, mnaelewana kwa undani?; Unamjua vipi mwenza wako? Hofu zake, vidonda vya utotoni, vitu vinavyomvunja moyo? Ukimya wao huashiria nini? Ukaribu wa kweli hujengwa kwa uaminifu na uwazi. Mnavyozidi kujuana ndipo mnapojitayarisha zaidi kupendana na kusapotiana kwa muda mrefu.

Je, mmeona upande wa kila mmoja katika nyakati tofauti za maisha?; Mtu anaweza kuwa mpole maisha yakiwa mazuri. Lakini je, anavyokabiliana na msongo, huzuni, uchovu, kuomboleza au hasira ni vipi? Kama mahusiano yenu mmeonana kwenye raha tu bado haujaona picha yenyewe, Maisha yatakufundisha mengi kuhusu mwenza wako.

Je, mnaweza kuzungumza kuhusu tendo la ndoa kwa uwazi?; Ikiwa urafiki wa kimwili ni sehemu ya ndoa yenu, mnaweza kulizungumzia kwa heshima bila aibu? Unategemea nini kutoka kwa mwenzi wako? Nini kinakufanya ujihisi salama?, Mipaka yako ni ipi?, Maongezi ya uwazi, uaminifu na heshima kuhusu tendo la ndoa ni kiashiria cha utimilifu. Mawasiliano haya ni muhimu kwa uhusiano wa kudumu.

Mnawezaje kusameheana?; Hakuna aliye mkamilifu. Lazima kuna kipindi mtakoseana, mtakwazana au utasema kitu kibaya. Je, mnaweza kusamehe? Unaweza kukiri makosa yako? Bila msamaha, chuki hujijenga haraka sana. Kwa msamaha, uponyaji huwezekana.

Upendo unaodumu ndani ya ndoa unaonekana katika mambo ya kawaida ya kila siku — jinsi unavyoongea ukiwa na hasira, kuchagua kusikiliza badala ya kufunga moyo, na kuendelea kutoa hata wakati hakuna hisia za kupenda.

Kufunga ndoa kwa sababu tu unampenda mtu ni kama kujenga nyumba juu ya mchanga. Inaweza kuonekana imara mwanzoni, lakini mtihani wa maisha utaiangusha ikiwa msingi wake ni hisia tu. Kwa hiyo, penda kwa moyo wote, lakini pia uliza maswali magumu. Jenga msingi. Jiandae. Kwa sababu pale ambapo upendo hautatosha, kile ulichojenga kuzunguka upendo ndicho kitawaweka pamoja.

“Uamuzi wa kufunga ndoa hautakiwi kufanywa kwa msingi wa hisia kali, bali kwa msingi wa maarifa.” — Dkt. Gary Chapman

Kwa hiyo, kama unasoma haya ukiwa bado hujapata mtu, usikimbilie mapenzi kwa presha ya umri au marafiki. Mtu sahihi anastahili kusubiriwa. Ni bora kuchukua muda kujenga kitu cha kweli kuliko kurukia kichwa kichwa kwenye kitu kilicho dhaifu. Haupo nyuma, unajenga kwa busara na hekima.

Kama upo kwenye mahusiano na unawaza kufunga ndoa, usikimbilie kwa sababu tu “unajisikia.” Toa muda. Uliza maswali ya kina. Jifunze mwenza wako kwa undani, jifunzeni jinsi mnavyobeba migogoro, presha, ukimya na mabadiliko. Upendo wa kweli unaweza kuvumilia uhalisia.

Na kama tayari umevishwa pete ya uchumba lakini unasoma haya ukihisi huzuni au mashaka, ni sawa. Bado hujachelewa kusimama na kutathmini upya. Ni bora kuuliza maswali magumu sasa kuliko kuyapotezea kwa kutegemea mambo yatabadilika baada ya ndoa. Kuahirisha au hata kukatisha uchumba si kushindwa — ni hekima. Inaonyesha unalichukulia jambo hili kwa uzito. Upendo unastahili uaminifu wa aina hiyo.

“Kuvunja uchumba ni bora kuliko kuvunja ndoa.” — Dkt. Gary Chapman

Ndoa haitatui matatizo, inayakuza.

Kama tayari umeoa au umeolewa, na maneno haya yanaonekana kama yanaelezea hali yako — usijisikie peke yako. Kila ndoa hufika mahali ambapo hisia hupungua na ule moto wa awali hauko tena kama mwanzo. Hii haimaanishi kwamba upendo umeisha; inamaanisha sasa ni wakati wa kuingia kwenye aina ya upendo wa kiutendaji. Upendo wa makusudi hauhitaji msisimko kila siku — unahitaji kujitokeza, hata siku ambazo ni ngumu. Uzuri ni kwamba siyo kuchelewa kujifunza tena, kuongea kwa kina, na kujenga upya kwa uimara zaidi. Ndoa si kuhusu ukamilifu — ni kuhusu kuchaguana tena na tena, siku za kawaida na hata zile zenye majaribu.

Upendo hautoshi, lakini hiyo si habari mbaya. Ni uhuru. Kwa sababu ukishajua kuwa ndoa inahitaji zaidi ya hisia, unaweza kuanza kujenga kitu thabiti, kitu cha kudumu. Usioe au kuolewa kwa sababu tu unampenda mtu. Funga ndoa kwa sababu uko tayari kukuza, kuhudumu, kujitoa, na kupendasiku ambazo ni rahisi, na hasa zile ambazo si rahisi.

Kwa upendo,

Sandrahope M.

Marejeo: Things I Wish I Knew Before I Got Married — Dkt. Gary Chapman


메타데이터
post_id
5c3aedfc0e5b
slug
ukweli-mgumu-kuhusu-upendo-na-ndoa-watu-wengi-huujua-wakiwa-wameshachelewa-5c3aedfc0e5b
url
https://medium.com/love-shack/ukweli-mgumu-kuhusu-upendo-na-ndoa-watu-wengi-huujua-wakiwa-wameshachelewa-5c3aedfc0e5b
canonical_url
https://medium.com/love-shack/ukweli-mgumu-kuhusu-upendo-na-ndoa-watu-wengi-huujua-wakiwa-wameshachelewa-5c3aedfc0e5b
author_url
https://medium.com/@SandrahopeM
status
ok
fetched_at
2026-06-26 03:39:16