KIBALI CHA UJENZI, UTARATIBU WA KUPATA, GHARAMA & MASWALI YAIHUSUYO.
Kibali cha Ujenzi (Building Permit) ni nyaraka ya kisheria inayotolewa na Mamlaka za Upangaji (Planning Authorities) ambazo ni Mamlaka za…
KIBALI CHA UJENZI, UTARATIBU WA KUPATA, GHARAMA & MASWALI YAHUSUYO.

Kibali cha Ujenzi (Building Permit) ni nyaraka ya kisheria inayotolewa na Mamlaka za Upangaji (Planning Authorities) ambazo ni Mamlaka za Serikali za Mitaa (The Local Government Authorities) ili kuruhusu Ujenzi mpya, kubomoa, kuondosha, kuongeza, au kufanya marekebisho makubwa.
Kisheria si ruhusa kwa mtu yeyote kujenga au kuanza kujenga jengo bila ya kuwa na;
- Uhalali wa umiliki wa ardhi mahali unapojenga.
- Kibali cha ujenzi kutoka mamlaka husika.
Katika makala hii tumegawanya vipengele vifuatavyo kwa ajili ya uelewa.
Uaharaka? SOMA HAPA KWA UFUPI
1. JINSI YA KUPATA KIBALI CHA UJENZI.
Unatakiwa kuwasilisha nyaraka zifuatazo:
- Michoro ya ramani ya jengo kwa ajili ya uchunguzi.
- Risiti/Slip ya benki ya malipo stahiki ya uchunguzi wa ramani hizo.
- Risiti au Slipu ya benki kwa malipo ya kiwanja kwa mwaka husika.
2. JINSI YA KUWASILISHA MAOMBI MICHORO YA MAJENGO MAALUMU.
Michoro ya majengo maalumu(Maghorofa, kumbi, Taasisi mbalimbali, Bar, Vituo vya mafuta, Viwanda, Hospital na majengo mengine ya jinsi hiyo iwasilishwe kwa kuanza na michoro ya awali ya kisanifu (Preminary Drawings) ambayo itahusisha.
- Michoro ya sakafu(Floor plan) 1:100
- Sura ya jengo(Elevations) 1:100
- Mkato wa jengo(Section) 1:100
Baada ya uchunguzi wa michoro ya awali kukamilika itawasilishwa michoro ya michoro (Final Drawings) ambayo ni michoro ya kisanifu na ya kihandisi(Architectural and structural drawings) kwa ajili ya uchunguzi.
● Michoro inayowasilishwa izingatie kanuni na taratibu zote muhimu za kiuchoraji(Architectural and Engineering Aspects) na iwe imesainiwa na msanifu majengo/Mhandisi anayetambuliwa(Architectural and Structural Endorsement). ● Michoro hiyo iambatane na nakala ya cheti cha uchunguzi wa athari za kimazingira(Environment Impact Assessment EIA). ● Michoro iambatane na nakala za nyaraka zote halali za umiliki wa kiwanja husika pamoja na stakabadhi ya malipo ya kiwanja kwa mwaka husika. ● Michoro yote iwasilishwe ikiwa na maandishi yanayosomeka(Readable text). ● Michoro yote iwasilishwe kwenye ukubwa wa karatasi(paper size) A0,A1,A2 au A3.
3. JINSI YA KUWASILISHA MAOMBI YA MICHORO YA MAJENGO YA KAWAIDA.
Michoro ya majengo ya kawaida itawasilishwa kwa kuzingatia maelezo ya hapo juu isipokuwa haitatangulizwa na michoro ya awali (Preminary Drawing) kama ilivyo katika michoro ya majengo maalumu.
4. MICHORO ILIYOANDALIWA IONYESHE NINI?
● Jengo litakavyokuwa(Plans, Sections, Elevations, Foundation,Roof plan,Site plan). ● Ramani ya kiwanja(Location plan). ● Namba na eneo la kiwanja kilipo. ● Jina la mmilikaji ardhi inayohusika. ● Jina la mchoraji, ujuzi na anuani. ● Ukubwa wa jengo kwa mita za mraba. ● Ujazo wa kiwanja(Plan ratio). ● Urefu wa jengo(Height). ● Matumizi yanayokusudiwa. ● Idadi ya maegesho yatakayokuwepo. ● Umbali kwa jengo kutoka kwenye mipaka ya kiwanja(Setbacks). ● Mfumo wa kutoa majitaka hadi kwenye mashimo.
5. VIAMBATANISHO UNAVYOTAKIWA KUWA NAVYO
● Fomu moja ya maombi iliyojazwa kwa usahihi.

● Fomu moja ya maombi iliyojazwa kwa usahihi.Hati ya kumiliki kiwanja au barua ya toleo. ● Kumbukumbu zingine zinazohusu kiwanja hicho kama hati za mauzo makabidhiano na mengine. ● Nakala ya risiti ya kodi ya kiwanja na kodi za majengo. ● Mabadiliko ya matumizi ya ardhi. ● Ramani ya kiwanja iliyosajiliwa.
6. TAHADHARI

Endapo mwananchi yeyote atajenga au kukarabati nyumba bila kibali cha ujenzi toka halmashauri, atapewa ilani ya kusimamisha ujenzi au ukarabati na kushauriwa kufuata taratibu za kuomba kibali cha ujenzi ndani ya siku 7. Kama mwombaji atakaidi ilani ya kusimamisha jiji au miji litampa ilani ya kubomoa jengo lake mwenyewe na akishindwa jiji litabomoa jengo husika na kudai mmiliki gharama za utekelezaji wa ubomoaji
....................................................................................................................
Je, uliwahi kufuatilia Kibali cha Ujenzi? Ulipitia hatua zipi na changamoto zipi? Una swali au nyongeza kuhusu Kibali cha Ujenzi? Karibu sana!
Mdau 1: Ahsante mkuu kwa mada. Hivi inachukua muda gani mpaka kupata kibali cha ujenzi?
Jibu: Ningependa kujibu kwa urefu swali hili:
Kwanza ifahamike wazi kuwa moja ya changamoto zinazokabili shughuli za Ujenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni pamoja na kuchelewa kutolewa kwa Vibali vya Ujenzi. Benki ya Dunia katika taarifa yake kuhusu urahisi wa kufanya biashara (Doing Business) ya Mwaka 2012 inaonesha kuwa katika kiashiria cha Vibali vya Ujenzi (Building Permits Indicator) nchini, mwombaji analazimika kupitia hatua kumi na tisa (19) na siku 303 ili kukamilisha hatua zote za maombi ya Kibali cha Ujenzi. Utaratibu huu si wa kuridhisha.
Hii ni tofauti na takwa la kisheria ambapo kwa kwa mujibu wa Kifungu cha 35 (i) cha Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya mwaka 2007, Mamlaka ya Upangaji inatakiwa kutoa kibali cha Ujenzi katika kipindi kisichozidi siku 60 kuanzia tarehe mwombaji alipowasilisha maombi yake. Aidha, ndani ya muda huo mamlaka inatakiwa kumjulisha mwombaji kuwa amekubaliwa au amekataliwa ombi lake na kutaja sababu zilizopelekea ombi lake kukataliwa.
Mwaka 2018 Serikali ilitoa mwongozo wa utoaji wa Vibali vya Ujenzi ambapo muda wa kukaa vikao vya kuidhinisha maombi ya Vibali vya Ujenzi umepunguzwa kutoka kufanyika kila baada ya miezi 3 mpaka (kila baada ya) wiki 2.
Kujibu swali lako sasa mkuu: Muda wa kutoa Vibali vya Ujenzi unatofautiana kutegemeana na aina ya jengo na ukubwa (complexity of the buildings) wa jengo. Ukaguzi unatakiwa kufanyika kwa umakini mkubwa. Jedwali hapa chini linaonesha muda wa kutoa Vibali kwa majengo tofauti.

Kwa ujumla ni kuwa: Endapo mwombaji atakamilisha hatua zote muhimu kwa wakati atapata kibali cha ujenzi ndani ya majuma mawili(2) hadi manne(4).Ahsante
Mdau 2: Ni sheria ipi inayosema ni lazima kuwa na kibali cha ujenzi mtu anapotaka kujenga? Kwenye post yako umesema tu 'Kisheria"…naomba tu kuelewa Dada, usinichoke.
Jibu: Hapana, siwezi kukuchoka ni wajibu wangu kuhakikisha unaelewa mada hii.
Sheria mbalimbali zimeeleza ulazima wa kuwa na Kibali cha Ujenzi.
Kwa mujibu wa Vifungu 124 na 125 vya Kanuni za Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Udhibiti Uendelezaji), Sura 288 (GN 242 ya mwaka 2008), Ujenzi wowote ndani ya Mamlaka za Upangaji ambazo ni Mamlaka za Miji Midogo, Halmashauri za Miji, Manispaa na Ma-jiji ni lazima upate kibali cha Ujenzi kutoka kwenye Mamlaka husika.
Mdau 3: Hivi document anayopewa mtu na mamlaka inayotoa vibali vya ujenzi baada ya kumaliza ujenzi wa jengo lake inaitwaje?
Jibu: Document inaitwa Certificate of Occupation au Cheti cha Kutumia Jengo kwa lugha ya Kiswahili.
Cheti hiki hutolewa baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa mwisho kwenye majengo ya maghorofa na majengo makubwa na wataalam wote wahusika ili kuhakikisha kuwa miundombinu na mifumo ya majitaka, maji safi, umeme, matumizi, barabara zinakidhi vigezo. Cheti kitatolewa na Halmashauri husika baada ya kuridhika na Ujenzi ulivyokamilishwa.
Mdau 4: Kwa hiyo mtoa mada kibali cha ujenzi hupatikana serikali za mtaa au office ya serikali ya mtaa?
Jibu: Ahsante kwa swali zuri. Kwanza, tujikumbushe kuwa kuna Serikali Kuu (The Central Government) na Serikali za Mitaa (The Local Government).
Pia ni vyema kufahamu kuwa kuna mifumo miwili ya Serikali za Mitaa, mfumo wa Mamlaka za Wilaya na ule wa Mamlaka za Miji.
Kibali cha Ujenzi hupatikana katika Mamlaka za Serikali ya Mtaa(Local Government Authorities). Hapa tunazungumzia Mamlaka za Upangaji (Planning Authorities) ambazo hupatikana katika Mamlaka za Halmashauri ya Wilaya na Mamlaka ya Mji (District & Urban Authorities).
Mdau 5: Hivi unalipia bei gani kupata kibali cha ujenzi wakuu?
Jibu: Mkuu, kwanza naomba ifahamike kuwa miongoni mwa changamoto zilizokuwepo katika utaratibu wa kutoa Vibali vya Ujenzi ni kutofautiana kwa gharama baina ya Halmashauri moja na nyingine.
Ili kutatua changamoto hiyo, Mwongozo wa Utoaji Vibali vya Ujenzi uliotolewa mwaka 2018 unaeleza kuwa Halmashauri zitoze ada za aina mbili:
- Ada ya ukaguzi (Scrutinization Fee) wa michoro ya jengo/majengo
- Ada ya Kibali cha Ujenzi (Building Permit Fee).
Ada hizo ni “non refundable” (hazirudishwi) na znatakiwa kulipwa kwa pamoja wakati wa kuwasilisha nyaraka za maombi ya kibali cha ujenzi. Pia ada hizi zinatakiwa kuzingatia vitu vifuatavyo;
- Ukubwa wa jengo na urefu wa jengo (Building Size and Height)
- Matumizi ya kiwanja husika (Land Use)
- Aina ya jengo (Type of Building))
- Ujazo wa kiwanja (Plot Coverage)
Kuhusu gharama halisi tuwasubiri wakuu wengine watakuja kuongezea nyama.
Mdau (Jibu): Kigamboni wana utaratibu wao, kuna sehemu nimeona hii taarifa ya 2019:
Mkurugenzi wa Kigamboni alitaja gharama za vibali vya ujenzi kwa maeneo ya makazi kuwa ni Sh 50,000 (mita za mraba 0–50), Sh 100,000 (mita za mraba 51–100) na Sh 150,000 (mita za mraba 101–150). Pia huko waliandaa michoro kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kwenda kuchora ambapo kwa nyumba ya vyumba viwili inauzwa Sh 30,000, vitatu (70,000) na vinne (150,000).
Mdau 6: Naomba kuuliza swali la nyongeza, hiki kibali cha ujenzi kibatolewa hata kwa viwanja vya uvamiz? maana unakuta katika viwanja vya uvamizi wale wanaouzianaga 50,000 kiwanja mtu akinyanyua kichumba chake kimoja au viwili et wanakuja kuandika maandish mekundu BOMOA, FIKA SERIKALI YA MTAA…Na ukienda wanakuuliza kibali cha ujenzi pale, na wanajua kabsa ni pa uvamiz.. Hili limekaaje wakuu??
Jibu: Mamlaka za serikali hawawezi kufahamu kama anayejenga ni mmiliki halali au sio mmiliki halali wa kiwanja japo wanaweza kufahamu kama kiwanja kimemilikishwa au la. Aidha ni muhimu kabla ya kuanza ujenzi, kuwa na kibali cha ujenzi hivyo ni wajibu wao kuandika maandishi hayo. Baada ya anayejenga kufika serikali za mtaa, ndipo inaweza kujulikana kama ni mmiliki halali au la, na vivyo hivyo kuchukuliwa hatua na mmiliki halali.
Hiki ni kipeperushi cha Halmashauri ya Temeke, kikielezea zaidi juu ya kibali cha ujenzi.
메타데이터
- post_id
- 64775eb656ca
- slug
- kibali-cha-ujenzi-utaratibu-wa-kupata-gharama-maswali-yaihusuyo-64775eb656ca
- url
- https://medium.com/@hamiahapa/kibali-cha-ujenzi-utaratibu-wa-kupata-gharama-maswali-yaihusuyo-64775eb656ca
- canonical_url
- https://medium.com/@hamiahapa/kibali-cha-ujenzi-utaratibu-wa-kupata-gharama-maswali-yaihusuyo-64775eb656ca
- author_url
- https://medium.com/@hamiahapa
- status
- ok
- fetched_at
- 2026-07-28 17:41:00