SHUKRANI JUU YA MAKALA YANGU YA MAHUSIANO BAINA YA CHINA NA TANZANIA
Moyo wangu umejaa shukrani kuweza kuwa mmoja wa waandishi wa Makala bora kupitia shindano lililoratibiwa na The Center for West African…
SHUKRANI JUU YA MAKALA YANGU YA MAHUSIANO BAINA YA CHINA NA TANZANIA

Moyo wangu umejaa shukrani kuweza kuwa mmoja wa waandishi wa Makala bora kupitia shindano lililoratibiwa na The Center for West African Studies (CWAS) of University of Electronic Science and Technology of China (Chengdu, Sichuan, P.R. China)
Makala yangu ilishiriki na kuwa moja ya makala bora katika “Essay competition: 2018 “China & Africa-China Friendship in My Eyes”.

Niliiona fursa hii kwenye moja ya makundi niliyomo ya We-Chat, miezi kadhaa iliyopita na moja kwa moja nikaisambaza kwenye makundi mengine, kisha mwenyewe kukaa na kuandika Makala yangu ya Mahusiano Baina ya China na Tanzania na kuiwasilisha kwa mamlaka husika.
Makala yangu pia ilikuwa sehemu ya mdahalo mkubwa wa Kimataifa wa masuala ya Utawala wa Umma 2018. “2018 International Conference on Public Administration pia katika kongamano la 2nd International Symposium on West African Studies” Midahalo hii ilifanyika hapo hapo kwenye chuo cha University of Electronic Science and Technology of China (Chengdu, Sichuan, P.R. China)Kwangu hii ni heshima na hatua kubwa ninayoichukulia kwa uzito wake

Ilikuwa nishiriki katika midahalo hii huko Sichuan Novemba Katikati, Chengdu- ila bado nilikuwa sijatengamaa baada ya operation niliyokuwa nimefanyiwa mwisho wa mwezi wa Oktoba. Nikawaeleza waandaaji kuhusiana uhalisia wa kwamba ningependa sana kushiriki ila nilihitaji kupumzika kwanza na kupona ili nirudi kuwa imara upya na wakasema wakimalizana na masuala yanyaohusu na mikutano hiyo watanitumia cheti na zawadi yangu katika mji niliopo wa Harbin, China.
Na wamefanya hivyo- kwangu ni baraka kubwa kwamba, wameuthamini mchango wangu, wamenithamini mimi. Na zaidi ya yote wameona kuwa nilichowasilisha kilikuwa na umuhimu, kilikuwa na thamani.
Yote haya ni kwasababu niliona kuwa mimi kama Mwanafunzi wa Kiafrika katika nchi hii ya China, ninapaswa kujitahidi kadri ya uwezo wangu niwe na muendelezo wa kushiriki kikamilifu fursa mbalimbali na katika kushiriki sio tu kuhudhuria mikutano au semina, fursa nyingine zipo kitaaluma zaidi; Kama hii ya Uandishi na zipo nyingine nyingi ambazo ni za kitaaluma zaidi.
Naamini bado ninahitaji kujinoa zaidi katika uandishi, ila naamini zaidi kuwa nina nafasi ya kujifunza kuandika vizuri kama nitaendelea kusikiliza ushauri ninaopewa na tathmini ninazopata juu ya makala zangu.

Kwa utii mkubwa ninaheshimu kuwa sehemu ya wahamasishaji wa vijana hapa nchini China juu ya masuala ya kuchangamkia Fursa, na kuwakilisha vema nchi yetu, kuwa mstari wa mbele kuinuana na kusaidiana, kupeana moyo ili kufikia malengo; tumekuwa na utaratibu huu chini ya Shirikisho letu la Watanzania wanaosoma China (TASAFIC) ambapo ninahudumu kama Makamu Mwenyekiti.
Naamini kuna nguvu kubwa katika kushirikiana na kuinuana, laiti kama mtu aliyekuwa na taarifa hii ya Chuo Hichi kuhitaji hizi makala kupitia shindano hili nililoshiriki- angeamua kutokutuma taarifa hiyo (aidha akawasilisha yeye mwenyewe) au akaipuuza tu, basi mimi leo hii nisingeweza kupaza sauti juu ya nchi yangu, na historia yake na ushirikiano wake na Uchina na hatimaye kuwasilisha makala iliyoingia kwenye Makala bora na kupata heshima hii siku ya leo.
Makala yangu kwa ufupi iligusia mahusiano kijumla ya China na Afrika, yaligusia pia, mahusiano ya Tanzania na China ambayo mwakani 2019 yatatimiza miaka 55, ni historia ndefu ambayo sasa inazidi kushika hatamu na hatuna budi kufahamu zaidi tulipotoka, tulipo na tunapoelekea na mahusiano/ushirikiano huu kiujumla.
Nilipokuwa naandika masala hii, nilidhamiria kuhakikisha kuwa Nchi ya Tanzania haikosekani kwenye washirki wa shindano hili, ila mwisho wa siku nchi yetu ya Tanzania, ikaonekana na kupewa tuzo kupitia mimi- hivi ndivyo nionavyo ushiriki wa masuala mbalimbali ya kimataifa- hujiwakilishi wewe tu, bali unawakilisha taifa lako kiujumla.
Ninachoomba kusisitiza ni kwamba, usiache kutuma fursa, usiache kuinua wenzako, huwezi jua utamuinua nani kupitia kumtaarifu mwenzako juu ya fursa fulani.
Nashukuru kila mmoja kwa salamu za pongezi na baraka, na heri.
Haya ni matokeo ya upendo, umoja na ushirikiano ambao tunapaswa kuudumisha.
Naamini huu ni mwanzo wa kuzidi kuinuana na kushirikiana.
Asanteni Sana
Victoria Mwanziva
🇹🇿🇹🇿🇹🇿🇹🇿🇹🇿🇹🇿🇹🇿🇹🇿
메타데이터
- post_id
- 96ba0a6715ee
- slug
- shukrani-juu-ya-makala-yangu-ya-mahusiano-baina-ya-china-na-tanzania-96ba0a6715ee
- url
- https://medium.com/@victoriacmwanziva/shukrani-juu-ya-makala-yangu-ya-mahusiano-baina-ya-china-na-tanzania-96ba0a6715ee
- canonical_url
- https://medium.com/@victoriacmwanziva/shukrani-juu-ya-makala-yangu-ya-mahusiano-baina-ya-china-na-tanzania-96ba0a6715ee
- author_url
- https://medium.com/@victoriacmwanziva
- status
- ok
- fetched_at
- 2026-07-29 21:02:00