← Back to list

Vita kati ya Netflix na Paramount katika kuinunua Warner Brothers na mustakabali wa burudani…

Kinachoendelea sasa kuhusu uwezekano wa kununuliwa kwa Warner Brothers Discovery ni kikubwa kuliko makubaliano ya kibiashara ya kawaida. Ni…

Ha Bib · 2026-06-01 06:01 · 3 claps · 4.4 min read
Open on Medium ↗
Wiki topics: SAF · Safety & Alignment 🎬 · Film & Television

Vita kati ya Netflix na Paramount katika kuinunua Warner Brothers na mustakabali wa burudani duniani

Kinachoendelea sasa kuhusu uwezekano wa kununuliwa kwa Warner Brothers Discovery ni kikubwa kuliko makubaliano ya kibiashara ya kawaida. Ni vita ya nani atapata mamlaka ya kuamua hatima ya ulimwengu wa burudani yenyewe. Nyuma ya vichwa vya habari, thamani ya mabilioni ya dola, na majadiliano ya kibiashara, kuna mgogoro mzito kuhusu nguvu, utamaduni, teknolojia, na mustakabali wa sinema. Sababu inayofanya sekta nzima kuitikia kwa hisia kali swala hili ni kwamba kila mtu anaelewa kuwa hili si suala la kampuni moja kununua nyingine tu; bali ni kuhusu kuamua Hollywood itakuwaje katika muongo mmoja ujao na pengine ni mambo gani yataacha kuwepo kabisa.

Warner Brothers Discovery si kampuni nyingine tu ya burudani iliyo kapuni ikisubiri mnunuzi. Inawakilisha moja ya nguzo za mwisho za nguvu za kitamaduni za Hollywood. Thamani yake haitokani tu na pesa au idadi ya waliojiunga na huduma zake za kidijitali, bali inatokana na miongo mingi ya kutawala sekta ya burudani na utamaduni.

Hii ndiyo studio iliyotengeneza baadhi ya hadithi zenye ushawishi mkubwa zaidi kuwahi kutokea. Kwa mfano, Batman si miliki ya kisanaa tu, bali imegeuka kuwa ni taasisi ya kitamaduni duniani kote. Harry Potter si mfululizo wa filamu tu, bali ni uzoefu wa kizazi kizima unaoanzia kwenye vitabu hadi viwanja vya mapumziko na burudani, bidhaa, na utamaduni wa mtandaoni. HBO ilibadilisha televisheni kwa kuthibitisha kuwa TV inaweza kubeba hadhi ya kisanii sawa na sinema kubwa. Game of Thrones ikawa moja ya matukio ya mwisho ya televisheni yaliyofuatiliwa na dunia nzima kila wiki. Hata mfululizo wa tamthilia za zamani kama Friends inaendelea kuingiza mabilioni kupitia kumbukumbu za watu na haki za urushaji. Warner Brothers Discovery inamiliki kumbukumbu, utambulisho, ushabiki, na uhusiano wa kihisia wa watu kwa kiwango kikubwa sana.

Hiyo ndiyo sababu kila mwekezaji mkubwa anataka sehemu ya kampuni hii. Lakini kinachofanya hali hii kuvutia zaidi ni kwamba kila mshindani anaitaka Warner Brothers kwa sababu tofauti, na sababu hizo zinaonyesha jinsi kila kampuni inavyouona mustakabali wa burudani.

Netflix inaiona Warner Brothers kama kipande cha mwisho kilichokosekana katika safari yake ya kutoka kuwa kampuni ya kiteknolojia iliyofanikiwa na kuwa himaya ya kudumu ya burudani. Netflix tayari inatawala soko la kidijitali (streaming) kwa ukubwa na ufikiaji wa kidunia, lakini imekuwa ikikosolewa kwa jambo moja: wingi wa maudhui haumaanishi kuwa na hadhi kubwa. Netflix inazalisha maudhui mengi yasiyoisha, lakini ni machache yanayofikia uzito au ubora wa kitamaduni wa muda mrefu ambao mali za HBO au Warner Brothers zinazo asilia.

Maudhui ya HBO yanahisiwa kuwa yameandaliwa, yamesukwa, na kukwezwa kwa namna ambayo bado inabeba hadhi ya kisanii. Netflix inaelewa kuwa ukuaji wa wateja utafika kikomo, na mara hilo likitokea, uwezo wa kuwabakiza wateja (retention) unakuwa kila kitu. Njia bora ya kubakiza wateja si kupitia wingi usioisha, bali kupitia maktaba ya filamu ambazo watu wanazipenda na kuzitegemea kihisia na kihistoria.

Hebu wazia unafungua Netflix na kukuta maktaba yote ya HBO imeunganishwa moja kwa moja kwenye jukwaa hilo, kando ya filamu za DC, kumbukumbu za Warner, maktaba ya Cartoon Network, na filamu zijazo za kwenye majumba ya sinema. Hilo lingebadilisha vita vya streaming ndani ya usiku mmoja. Netflix isingekuwa tu huduma kubwa zaidi ya streaming; ingekuwa nguvu kuu ya burudani yenye uzito wa kitamaduni usio na mpinzani. Hii si kuhusu kupata maudhui tu; ni kuhusu kupata uhalali, hadhi, na udumu.

Kinachofanya nafasi ya Netflix kuwa ya kuvutia zaidi ni kwamba ununuzi huu unakwenda kinyume na mkakati wao wa kawaida. Netflix ilijenga himaya yake asilia (organic). Kwa mara chache sana Netflix ilishiriki katika miungano mikubwa ya makampuni (mergers) kwa sababu inapendelea kudhibiti mfumo wake yenyewe kutokea ndani. Ndiyo maana uwezekano huu wa kuinunua Warner Brothers unaashiria hali ya kukata tamaa sawa na ilivyo na tamaa ya madaraka. Netflix inaelewa kuwa vita vya streaming vinaingia katika awamu mpya. Ukuaji unapungua. Wateja wanazidi kuwa na uchaguzi mgumu. Ushindani si kuhusu kuwa na bei rahisi tena, bali ni kuhusu kumiliki maudhui yenye thamani kubwa zaidi ya kihisia na kibunifu. Warner Brothers inatoa jambo hilo kwa usahihi.

Nia ya Comcast inaonyesha upande mwingine wa biashara ya habari ya baadaye. Comcast tayari inamiliki Universal na NBC, ikimaanisha kuwa kuinunua Warner Brothers kungetengeneza mashine kubwa ya burudani iliyounganishwa kila upande (vertical integration). Hawafikirii kuhusu streaming pekee; wanafikiria kuhusu “mifumo ya kimaisha” (ecosystems). Kila mhusika wa Batman anakuwa kivutio kwenye maeneo ya burudani.

Kila miliki ya HBO inakuwa bidhaa adhimu, uzoefu wa kibiashara, leseni, na uingizaji wa pesa kupitia majukwaa mbalimbali. Makampuni ya kisasa ya habari hayaingizi pesa kupitia filamu na TV pekee; yanaingiza pesa kwa kugeuza hadithi kuwa ulimwengu mzima ambao wateja wanaweza kuingia kimwili na kujiingiza kifedha kwa miongo mingi.

Kisha kuna Paramount na familia ya Ellison, ambao ushiriki wao unageuza jambo hili kutoka majadiliano ya kawaida ya kibiashara na kuwa kitu kinachokaribia siasa na utawala wa kifamilia (dynastic). Larry Ellison ni mmoja wa watu matajiri na wenye nguvu zaidi duniani, na watu wa kiwango hicho mara chache hukubali kushindwa kiungwana.

Mkakati wa Paramount ni tofauti kwa sababu wanajaribu kutengeneza muungano wa makampuni ya habari yenye uwezo wa kusimama dhidi ya utawala wa kiteknolojia wa Silicon Valley. Katika mambo mengi, hoja ya Paramount ni ya kiitikadi; kimsingi wanasema kuwa makampuni ya asili ya Hollywood yanahitaji kuungana ili yaweze kuishi dhidi ya wababe wa kiteknolojia kama Netflix, Amazon, Apple, YouTube, na TikTok.

Akina Ellison pia wanawakilisha aina mpya ya nguvu ya Hollywood. Hollywood ya zamani iliongozwa na wakuu wa studio waliojifunza kazi ndani ya mifumo ya burudani. Hollywood mpya inazidi kutengenezwa na mabilionea, wawekezaji, makampuni ya mitaji binafsi, na wajasiriamali wa teknolojia. Mabadiliko hayo yanabadilisha kila kitu kwa sababu uandishi wa hadithi unakuwa na uhusiano mkubwa na ufundi wa kifedha (financial engineering) kuliko utambulisho wa kisanii. Paramount Skydance yenyewe ilitokana na muungano tata uliokuwa na uungwaji mkono mkubwa wa kitaasisi. Wana uzoefu wa kuendesha dili kubwa, vita vya kisheria, na miungano ya wawekezaji. Netflix inaweza kuwa na pesa, lakini akina Ellison wana mahusiano ya kisiasa, uungaji mkono wa kitaasisi, na uzoefu wa ununuzi mkali wa makampuni.

Ushiriki wa mifuko ya utajiri wa nchi za kigeni (Sovereign Wealth Funds) kutoka Mashariki ya Kati unaongeza sura nyingine kabisa, ukionyesha jinsi umiliki wa burudani ulivyokuwa wa kidunia (globalized). Hollywood ilikuwa ikimwakilisha mtawala wa kitamaduni wa Marekani; sasa Hollywood yenyewe inazidi kutegemea mitaji ya kimataifa ili kuishi. Ukweli huo unaleta matatizo ya kisheria kwa sababu uwekezaji wa kigeni unapoingia, wasiwasi kuhusu ushawishi, maslahi ya taifa, na udhibiti unakuwa suala nyeti sana kisiasa. Burudani haitazamwi kama biashara tu tena; serikali zinaelewa kuwa vyombo vya habari vinatengeneza utamaduni, hadithi, na hata uelewa wa kisiasa wa watu. (Itaendelea ….)

Usikose sehemu ya pili ya mfululizo wa mada hii. Hakikisha unaacha maoni, kulike, kutumia marafiki na wadau wengine kujifunza. Tusaidie kufikisha mada hizi kwa watu wengi zaidi wanaotaka kujifunza mambo mbalimbali ya filamu.


메타데이터
post_id
c36fd0428595
slug
vita-kati-ya-netflix-na-paramount-katika-kuinunua-warner-brothers-na-mustakabali-wa-burudani-c36fd0428595
url
https://medium.com/@Ha_Bib/vita-kati-ya-netflix-na-paramount-katika-kuinunua-warner-brothers-na-mustakabali-wa-burudani-c36fd0428595
canonical_url
https://medium.com/@Ha_Bib/vita-kati-ya-netflix-na-paramount-katika-kuinunua-warner-brothers-na-mustakabali-wa-burudani-c36fd0428595
author_url
https://medium.com/@Ha_Bib
status
ok
fetched_at
2026-06-24 04:09:36