← Back to list

Kukaa kwa Wazazi au Ghetto

Utamsikia mtu anakwambia "Oya, kukaa nyumbani kwenu ni umama!" Mwingine anakwambia "Mwanamke kuchakarika, utakaaje kwa wazazi? Toka…

Luckson Massatu · 2021-02-20 15:33 · 0 claps · 2.1 min read
#lifestyle #hustler #hustlers-2019
Open on Medium ↗
Wiki topics: ✨ · Lifestyle · General 👗 · Fashion

Kukaa kwa Wazazi au Ghetto

Utamsikia mtu anakwambia "Oya, kukaa nyumbani kwenu ni umama!" Mwingine anakwambia "Mwanamke kuchakarika, utakaaje kwa wazazi? Toka nyumbani ingia mjini kaa peke yako ndo akili zitakuja!" Swali la msingi hapa ni hili; anajua kwa nini bado uko kwenu? Japo kuna ukweli kiasi katika kauli zote hizi mbili, leo nataka nikwambie ukweli mwingine.

Zipo faida na hasara nyingi za kukaa kwa wazazi wako hata kama umefikia umri wa kujitegemea. Faida na hasara hizi zinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hata mwingine kulingana na malezi, mazingira, malengo ya mtu husika, mahitaji yake, imani na itikadi zake binafsi.

Ukimuuliza kijana ambaye anaishi kwa wazazi wake ingawaje amefikia umri wa kujitegemea atakupa sababu zake. Tena inawezekana kabisa kijana huyu asiwe na mpango wa kuamua kutafuta kwake hivi karibuni. Vivyo hivyo kwa kijana mwenye kwao lakini anaishi ghetto.

Katika kufanya maamuzi ni lazima uhusianishe maamuzi yako na malengo yako uliyojiwekea. Kama huna malengo kabisa, nasikitika kukwambia kuwa maisha yatakuwa magumu kwako mpaka unaingia kaburini. Kinyume chake ndicho ninachokushauri sasa. Malengo yako ndiyo msingi wa maamuzi yako. Malengo yako ndiyo yatakayokuruhusu kuamua kukaa kwa wazazi au kutoka na kujitegemea.

Jambo la muhimu kuzingatia wakati wa kuweka malengo yako ni muda. Hakuna malengo yasiyotambua kipengele cha muda. Ukisema "Nitaka kabla ya mwaka huu kuisha niwe nimenunua kiwanja". Mwaka ni muda. Yupo mtu anayeishi kwa wazazi wake hadi leo kwa sababu ndipo mahali pekee anapoweza kupatumia kutimiza lengo lake la kununua kiwanja ndani ya muda aliojiwekea. Sababu inaweza kuwa gharama za kodi ya nyumba, ambayo angelipia kama akikaa kwake, anaihamishia kwenye bajeti ya kiwanja. (Huu ni mfano). Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanafahamu kuwa ili kutimiza lengo ulilo nalo ni busara kutumia mbinu zitakazokugharimu kidogo.

Usipelekwe na mawazo ya watu wengine kuhusu mambo yanayokuhusu wewe mwenyewe. Vijana walio wengi, hasa wa jinsia ya kiume hivi sasa wanaamini na kuaminishana kuwa ni fedheha kwa kijana aliyetimiza umri wa kujitegemea (miaka 20+) kuendelea kuishi kwa wazazi. Wengine wanakwenda mbali na kutoka kwa wazazi wanaoweza kuwasaidia kwa namna fulani na kupanga vyumba ili tu aonekane naye "anahustle". Matokeo yake anaishia kujilimbikizia madeni kuanzia kwa ndugu, marafiki mpaka kwa mama ntilie.

Kuanza kutafuta kujitegemea mapema ni jambo jema pia lakini linapaswa kufanyika baada ya kuchakata machaguo na fursa nyingine zilozopo. Usiamue jambo kwa namna fulani kwa sababu vijana wenzako wote wanamua kwa namna hiyo. Jambo sahihi sio lazima lifanywe na watu wengi. Zingatia kuwa, Njia unayoipita wewe katika maisha yako ni matokeo ya maamuzi yako. Maamuzi yako ni matokeo ya malengo yako. Malengo yako yanatokana na imani, itikadi na mazingira uliomo au ulimokulia. Hivi vyote ukivichunguza kwa umakini utagundua kuwa hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, sasa kwa nini ujifananishe na yule?

Kama kukaa kwa wazazi kutakusogeza karibu na ndoto zako kwa urahisi, itumie fursa hiyo huku lengo likiwa wewe kusimama peke yako siku moja. Kama kukaa kwa wazazi kutakuchelewesha, ondoka, nenda njia inayolandana na malengo yako. Usiwaruhusu watu wakuharakishe na mipango yao. Wewe sio wao na wao sio Mungu. Mtangulize M/Mungu.

Kila la Kheri.


메타데이터
post_id
cf6063d9f09e
slug
kukaa-kwa-wazazi-au-ghetto-cf6063d9f09e
url
https://medium.com/@massatuluckie/kukaa-kwa-wazazi-au-ghetto-cf6063d9f09e
canonical_url
https://medium.com/@massatuluckie/kukaa-kwa-wazazi-au-ghetto-cf6063d9f09e
author_url
https://medium.com/@massatuluckie
status
ok
fetched_at
2026-08-01 17:11:43