MAMBO AMBAYO NITAMFUNDISHA BINTI YANGU.
Naogopa kuhusu wanaume ambao watajaribu kumtreat kama mzigo, kumtumia kama kitu tu, na kumwacha. Nina wasi wasi pindi ambapo atakapoondoka…
MAMBO AMBAYO NITAMFUNDISHA BINTI YANGU. _ Leo wasichana wana chaguo zaidi zaidi kuliko walizokuwa nazo zamani, na kuna ushawishi mkubwa zaidi katika maisha yao, Naogopa kuhusu binti yangu.
Naogopa kuhusu wanaume ambao watajaribu kumtreat kama mzigo, kumtumia kama kitu tu, na kumwacha. Nina wasi wasi pindi ambapo atakapoondoka kwangu, kutakua na muda nyota haitakua upande wake kwa mazuri, na wengine watatumia mwanya huo. Dunia iko kimya sana kuhusu mabinti zetu, Mimi nitamfundisha na kumkumbatia vilivyo na nitajaribu, nitajaribu kumlinda, kumpooza, kumpooza kwa maumivu yake na maumivu ya moyo.
Siku za hivi karibuni nimesikia kuhusu case ya mwanamke mmoja ambae aligeuka kuwa mtafutaji mkuu katika familia. Hili lilikuja baada ya baba kuhamia kwa mke mwingine aliyemuoa hivi punde akasahau kabisa mke wake wa kwanza!
Mwanamke yule akafunga kanga yake vizuri na kuanzisha biashara yake. Biashara ikamea ingawa wanafiki hawakosi siku zote, stori juu ya kwamba mafanikio ya biashara ile ni fedha za wanaume wanamuhonga zilienea na kumpalilia Mme ambae kwa kipindi hiko alikua akijirudi baada ya kuyaona mafanikio.
Siku moja Mme mtu aliona meseji ya utani kati ya mke na mteja wake...ukawa ugomvi_alimpiga, akamtupa juu ya fensi na kumsababishia umauti mwanamke wa watu!
Hii sio dunia ninayotaka kuiona kwa binti yangu. Nimeshaona taarifa kama hizi kwenye vyombo vya habari kabla. Nazijua stori hizi. Nitamwambia juu ya bibi yake alivyotumia fagio kujitoa mikononi mwa babu yake kwenye ugomvi ambao Mimi sikuusogelea kabisa licha ya kwamba ilikua wazi nilimjua mwenye kosa nani.
Nitamwambia mengi, huku nikimwangalia machoni pake, nini dunia itahitaji kutoka kwake, na nini itajaribu kuchukua kutoka kwake.
Dunia itajifanya inampa mwangaza fulani, hapo hapo akikaribia tumaini itampindua chini na kumkabidhi kiza, kiza kama kile cha kwenye korido za nyumba za Temeke Mikoroshini. Hapo atahitaji nguvu yake binafsi kujikwamua.
Nguvu yake binfsi ndio nitahitaji kumfundisha. Nitataka mwanamume aache kiti chake kwa ajili yake. Nitaomba kwa Mungu kwamba ataziacha nywele zake mtindo autakao au atengeneze Peruvian Hair kivyovyote nakusiwepo na athari ya namna yeyote kwenye interview!,
Natamani binti yangu ndoto zake zisizibwe na kiwembe mdomoni kwake, Yale maneno makali makali kutoka kwa mama yake, nitayachuja na kumfanya awe salama pale ambapo dunia itakapojaribu kuingilia na kumtafutisha yeye na moyo wake.
Yaani nitam-BOLD na Kum- ITALIZE atakayekuwa binti yangu. Atajua tu kwa yeye ni hadifainiki na hakataliki!
Nitamfundisha kwamba historia ya watu wake imeandikwa kama tatoo kwenye udongo wa mifupa yake. Stori za Nyung'u-ya-mawe, Kayagwa, Bilalama na Kitumba kuwa ndio urithi wake mkuu. Na nitamweka mbali na mambo ya ubaguzi. Yeyote amfanye rafiki na kuukuza ukoo. Nitamsisitizia ya kuwa ufalme huundwa na watu.
Nitamwambia kuhusu nyumba za kwenye miti na viota vya ndege na ya kwamba nguvu ya mvutano wa kidunia maarufu kama gravitational force, sio kila kitu! Mungu ndio kila kitu, ya kwamba ataweza hata kuruka angani akimtumainia Mwenyezimungu.
Nitaruka mbele yake kumkinga na risasi na machine yeyote itakayotengenezwa kudhamiria kumlenga.
Nitamwelekeza ya kwamba paradiso yake iko kwenye urefu wa mikono yake, kifundo cha mguu cha mababu zake, kipande cha nguo kilichotunza kitovu cha uchanga wake. Kwamba sura yake imeundwa na tabasamu la kiha, kwamba mwanga na damu ni maji ya bahari na yanaendeshwa na yeye! Yeye Peke Yake.
Kwamba yajayo hayako kwenye nyimbo za kama za Wasafi, yajayo yako kwake tu, alpha na omega.
Baba yake nataka yeye awe chochote atakachokitaka. Kwamba haihitaji definition yoyote, au maazimio yoyote, kwamba atakuwa raisi au mbunge au mama au maua au superhero au mwandishi au nyumbani tu.
Ndio, atakua nyumbani kijijini kwenye asili lazima afike na aishi. Uwepo wake, nitamwambia inabidi uwe mzito! Wenye ujazo na mguso.
Waambie Mabinti wote nimewaambia haya.
Mwisho.
메타데이터
- post_id
- 55eb4fe796db
- slug
- mambo-ambayo-nitamfundisha-binti-yangu-55eb4fe796db
- url
- https://medium.com/@Baloziwamitaa/mambo-ambayo-nitamfundisha-binti-yangu-55eb4fe796db
- canonical_url
- https://medium.com/@Baloziwamitaa/mambo-ambayo-nitamfundisha-binti-yangu-55eb4fe796db
- author_url
- https://medium.com/@Baloziwamitaa
- status
- ok
- fetched_at
- 2026-07-27 19:47:14